Rais wa Senegal Bassirou Diomaye Faye Jumanne alimuagiza waziri wake mkuu kuandaa “mpango wa dharura” wa kuimarisha uchumi na sekta ya fedha iliyo katika hali ngumu nchini humo, ofisi yake ilisema katika taarifa.
Rais huyo mwenye umri wa miaka 44 alipata ushindi wa kishindo katika uchaguzi wa mwezi uliopita kwa ahadi ya mageuzi makubwa, na kuwa rais mwenye umri mdogo zaidi licha ya kuwa hakuwahi kushikilia wadhifa wa kuchaguliwa.
Jumanne, alimpa waziri wake mkuu na mshirika wake wa karibu Ousmane Sonko muda wa hadi mwishoni mwa mwezi huu kuandaa “mpango madhubuti”, ilisema taarifa hiyo iliyotolewa baada ya mkutano wa kwanza wa baraza lake la mawaziri.
Alimuagiza Sonko “kufanya tathmini ya jumla ya programu na mipango” na kutoa ripoti kuhusu hali ya jumla ya fedha za umma”, ushirikiano wa kimataifa na ushirikiano wa sekta ya umma na binafsi, taarifa hiyo ilisema.