Poland imewakubali zaidi ya wakimbizi wa Ukraine milioni 2.
Hakutakuwa na sitisho la mapigano au maridhiano yoyote kwa Russia, mpatanishsi mkuu kwa Ukraine alisema Jumamosi wakati Russia ikiongeza mashambulizi huko. Luhansk, moja ya majimbo mawili yanayounda eneo la Donbas huko Ukraine mashariki.
“Vita hivi havitasita (baada ya maridhiano). Vitasimamishwa kwa muda fulani,” Mykhailo Podolyak, ambaye pia ni mshauri wa Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy, alisema, akielezea msimamo wa Ukraine kufuatia wito wa kuwepo sitisho la mapigano kutoka kwa Waziri wa Ulinzi wa Marekani Lloyd Austin na Waziri Mkuu wa Italia Mario Draghi.
“Wataanza mashambulizi mapya, ambayo yatakuwa na umwagaji damu zaidi na makubwa,” Podolyak aliongeza kusema.
Wanaotaka kujitenga wanaoungwa mkono na Russia wamekuwa wanapambana na Ukraine ili kudhibiti majimbo ya Luhansk na Donetsk – ambayo yanaunda Donbas – tangu mwaka 2014, wakati Russia ilipoiteka Rasi ya Crimea.
Majeshi ya Ukraine katika majimbo hayo mawili imesema kupitia mtandao wa Facebook kuwa takriban watu saba walikuwa wameuwawa huko Donetsk katika kipindi cha saa 24 wakati Warussia wakitumia ndege, mizinga, vifaru, roketi, mabomu na makombora, walishambulia majengo na makazi ya raia, Reuters imeripoti.
Waukraine walisema walikuwa wamezuia mashambulizi tisa, wameharibu vifaru vitano na magari ya kivita 10, kulingana na ujumbe wao wa Facebook.
“Hali huko Donbas ni ngumu sana,” Zelenskyy alisema Jumamosi katika hotuba yake ya usiku. Alisema majeshi ya Ukraine yamelizuia jeshi la Russia wakati likijaribu kushambulia miji ya Sloviansk na Sievierodonetsk.
Katika maendeleo mengine Jumamosi, Russia imechapisha orodha ya karibu Wamarekani 1,000 ambao wamepigwa marufuku kabisa kuingia Russia kwa sababu ya kuiunga mkono Ukraine.
Rais Joe Biden na Makamu wa Rais Kamala Harris ni kati yao walioorodheshwa wakiwemo wajumbe wa Baraza la Mawaziri la Rais.