Lakini, katika ishara ya mzozo ambao unaweza kutokea, rais wa zamani anayekabiliwa na kashfa ya rushwa Jacob Zuma alisusia hafla ya kutangaza matokeo na chama chake kilichopata nafasi ya tatu cha uMkhonto weSizwe (MK) kilikataa kukubali matokeo.
Hesabu ya mwisho ya kura ilikipa chama tawala cha Ramaphosa cha African National Congress viti 159 katika bunge la taifa lenye viti 400, ushindi wake wa chini kabisa katika uchaguzi mkuu.
Chama cha upinzani cha mrengo wa kati cha Democratic Alliance (DA) kilipata viti 87, MK cha Zuma kilipata viti 58 na chama cha Julius Malema cha Economic Freedom Fighters (EFF) kilipata viti 39, kikifuatiwa na vyama kadhaa vidogo.
Chama hicho cha kiongozi mkombozi wa taifa hayati Nelson Mandela kilipata zaidi kidogo ya asilimia 40 chini ya asilimia 57 kilichopata mwaka 2019.
Bunge jipya litakutana ndani ya wiki mbili na kazi yake ya kwanza itakuwa kumchagua rais atakayeunda serikali mpya.
Lakini kwa sababu hakikupata ushindi wa kutosha kwa mara ya kwanza tangu ujio wa demokrasia baada ya enzi ya utawala wa ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini, ANC kitalazimika kutafuta uungwaji mkono wa vyama vingine ili Ramaphosa achaguliwe kwa muhula mwingine.