Kwa mujibu wa taarifa ya ikulu iliyotolewa Jumapili imeeleza kuwa kipindi chake Profesa Assad cha miaka 5 katika nafasi hiyo kinaisha leo saa sita usiku.
Akizungumza baada ya uapisho huo wa CAG mpya ulioenda sambamba na watendaji wengine aliowateua, Rais Magufuli amemkumbusha CAG mpya aliyeteuliwa kwamba yeye si muhimili wa serikali bali ni mtumishi tu.
Amemkumbusha kuwa anapaswa kupokea maelekezo kutoka kwa mihimili iliyopo yaani serikali, bunge na mahakama.
Profesa Assad ameviambia vyombo vya habari ingekuwa bora watu wengine wakafafanua juu ya uamuzi huo kwani ni hatua ya kisheria, kwa kuwa suala hilo linafungamana naye.
Alieleza jana anatarajia Jumatatu kupatiwa barua yake rasmi kwa kuwa uteuzi ulifanyika mwishoni mwa juma na haikuwa wakati wa kazi.
Amesema ataamua hatua gani achukue pale atakapopokea barua rasmi itakayo nukuu vifungu ambavyo vinafanya aondolewe madarakani na ana njia nyingi za kukabiliana na uamuzi huo.
''Jambo hili si la kisiasa ni jambo la kisheria, lakini nasema riziki anayo mwenyewe Mwenyezi Mungu..., kuna vitu chungu nzima za kufanya Inshallaah, Mungu atatufanyia wepesi na kila kitu kitakwenda vizuri.'' alieleza Profesa Assad.
CAG Assad anayeondoka madarakani aliigia katika mgogoro mkubwa na Bunge kwa kile Spika Job Ndugai alichokiita kulidharau bunge hilo kwa kuliambai ni dhaifu, na hivyo bunge kupitisha azimio la kukataa kufanya kazi na Profesa Assad.
Kadhalika Rais amemtaka pia CAG mpya Kichere kusafisha ofisi yake kwani kuna matumizi mabaya ya fedha.
Naye Spika wa bunge Job Ndugai alimwelezea CAG mpya namna ambavyo Bunge linahitaji ushirikiano wake.
Imetayarishwa na Mwandishi wetu, Washington, DC.