Rais Biden atetea mafanikio yake katika sera ya kigeni

Biden akizungumza kuhusu sera ya kigeni katika hotuba kwenye wizara ya mambo ya nje ya Marekani, Januari 13, 2025. Picha ya AP

Rais Joe Biden anayekamilisha muhula wake Jumatatu alipongeza rekodi yake ya sera ya kigeni akisema wapinzani wa Marekani wamekuwa wadhaifu kuliko kipindi alipoingia madarakani miaka minne iliyopita, licha ya mizozo ya kimataifa ambayo bado haijatatuliwa.

Wiki moja kabla ya kumkabidhi madaraka Rais mteule Donald Trump, Biden katika hotuba nadra kwenye wizara ya mambo ya nje alipongeza uungaji mkono wa utawala wake kwa Ukraine dhidi ya uvamizi wa Russia wa mwaka 2022 na kwa vita vya Israel katika kanda ya Mashariki ya Kati.

Biden alisema Marekani “imeshinda katika ushindani duniani kote” na haitokuwa nyuma ya China kiuchumi kama ilivyotabiriwa, huku Russia na Iran zikiwa zimedhoofishwa na vita bila ushiriki wa moja kwa moja wa Marekani.

“Ikilinganishwa na miaka minne iliyopita, Marekani ina nguvu zaidi, washirika wetu wana nguvu zaidi, maadui na washindani wetu ni wadhaifu,” Biden alisema.

“Hatukwenda vitani ili kufanya mambo hayo yawezekane.”

Biden alisema aliisaidia Israel kuwashinda maadui kama Hamas huko Gaza na Hezbollah nchini Lebanon, makundi yote hayo yakiungwa mkono na Iran.

Rais wa Marekani amepongeza pia msaada wa Washington kwa Israel wakati wa mashambulizi mawili ya Iran mwaka 2024.