Raia watatu wameuawa na wengine 20 kujeruhiwa katika shambulizi la ndege isiyo kuwa na rubani lililofanywa na wanamgambo katika mji wa magharibi mwa Sudan wa El-Fasher huko Darfur Kaskazini, maafisa wamesema Jumapili.
Kundi la watu wa kujitolea limesema katika taarifa kwamba shambulizi hilo lilifanyika Jumamosi usiku.
Limesema kikosi cha wanamgambo cha Rapid Support Forces (RSF) ambacho kimekuwa kikipigana na jeshi la serikali tangu Aprili mwaka 2023, kililenga “kitongoji cha Awlad al-Reef katikati mwa mji kwa makombora manne, na kuua raia watatu na kujeruhi wengine zaidi ya 20 ambao walipata majeraha mabaya.”
Mji wa El-Fasher umekuwa chini ya udhibiti wa RSF tangu mwezi Mei.
Mji huo umekuwa uwanja wa mapigano makali huku pande zote zikitaka kuudhibiti.