Putin alisafiri hadi Vietnam, mshirika wa karibu wa Moscow tangu enzi za Vita Baridi, kutoka kwa mkutano mkuu na Kim Jong Un wa Korea Kaskazini, ambapo Kim aliahidi "uungaji mkono kamili" kwa Russia katika vita vyake dhidi ya Ukraine na wawili hao kutia saini mkataba wa ulinzi wa pande zote. Kiongozi wa Russia hakupata hakikisho la wazi kama hilo, la uungaji mkono kutoka Hanoi, lakini Rais wa Vietnam To Lam alionyesha ari ya kuimarisha ushirikiano wa kiulinzi.
"Pande zote mbili zinataka kuhimiza ushirikiano katika ulinzi na usalama, jinsi ya kukabiliana na changamoto za kiusalama kwa misingi ya sheria za kimataifa, kwa ajili ya amani na usalama duniani," Lam aliwaambia waandishi wa habari baada ya mazungumzo na Putin.