Ongezeko kubwa la wahamiaji wanaovuka mpaka kuingia Marekani lazua wasiwasi

Wahamiaji wanaojaribu kuingia Marekani.

Idara ya  uhamiaji ya Marekani Alhamisi iliripoti ongezeko kubwa la watu wanaovuka mpaka wa kutoka Mexico kuingia Marekani kinyume cha sheria, hasa katika maeneo kama Eagle Pass, jimbo la Texas, ambapo meya wa mji huo ametangaza hali ya tahadhari.

Maafisa wa Doria ya Mipaka ya Marekani waliwakamata wahamiaji wapatao 9,000, kwenye mpaka huo, katika muda wa saa 24, kulingana na ripoti za vyombo vya habari.

Sauti ya Amerika iliauliza maafisa wa kulinda mipaka iwapo wangethibitisha idadi hiyo, lakini afisa mmoja, , alisema wanasubiri kutoa idadi yao katika ripoti ya kila mwezi.

Ongezeko linaloonekana la wahamiaji waliofika katika Eagle Pass liliongeza changamoto kwa rasilimali za ndani, na hasa kwa vituo ambavyo tayari vilivyokuwa vimejaa watu.

Siku ya Jumatano jioni kati ya wahamiaji 500 na 800, wengi wao kutoka Venezuela, walikuwa wakisubiri kushughulikiwa na maafisa wa Doria ya Mpakani, chini ya Daraja la Kimataifa la Eagle Pass-Piedras Negras, mojawapo ya madaraja mawili katika Eagle Pass.