Obama: Dunia iko salama zaidi baada ya kifo cha Bin Laden

Obama Bin laden

Maafisa wamekaririwa wakisema vipimo vya DNA vilitoa makadirio ya asilimia 99.9 kwa hakika ni kwamba Bin Laden amekufa.

Rais Barack Obama anasema dunia iko katika hali ya usalama zaidi baada ya kifo cha kiongozi wa al-Qaeda Osama bin Laden.

Akizungumza White House Jumatatu Bw. Obama alisema ni “siku nzuri kwa Marekani” na kwamba Marekani imetimiza ahadi yake kuona haki imetendeka.

Rais alitangaza Jumapili usiku mjini Washington kwamba Bin Laden ameuwawa na majeshi ya Marekani ndani ya nyumba moja huko Pakistan.

Maafisa wamekaririwa wakisema vipimo vya DNA vilitoa makadirio ya asilimia 99.9 kwa hakika ni kwamba Bin Laden amekufa.

Bw. Obama alisema Jumapili kuwa kikosi kidogo cha wamarekani kilifanya shambulio hilo lililopangwa kwenye nyumba huko Abobottanad eneo la matajiri kaskazini mwa Islamabad.

Amesema majeshi ya Marekani yalimuuwa Bin Laden baada ya mapigano na kusema amezikwa na majeshi ya Marekani baharini kutoka kwenye meli ya kivita ya Marekani katika bahari ya Arabia. Wanasema mwili wake ulihifadhiwa kwa kanuni zote za dini ya kiislam.

Bw. Obama aliita kitendo hicho kuwa ni mafanikio makubwa kuliko yote katika mapambano ya kuwashinda al-Qaeda na kusema hakina budi kupokelewa na wote wanaopenda amani na heshima ya binadamu.

Katika mkutano na waandishi wa habari White House imeelezea kuwa operesheni hiyo ilikuwa ngumu na hatari . Afisa mmoja amesema Marekani haikushirikiana kutoa habari hiyo juu ya shambulizi na nchi yeyote na hata katika serikali ni wachache sana waliojua mapema juu ya mpango huo.

Kuuwawa kwa Bin Laden kumetokea karibu mika 10 baada ya mashambulio ya Septemba 11,2001. Karibu watu 3000 waliuwawa katika shambulio hilo.