Nigeria: Watu 61 watekwa nyara na washambuliaji wenye silaha

Picha hii inayonyesha wazazi wakisubiri kupata taarifa kuhusu watoto wao waliotekwa nyara katika shule ya sekondari na msingi huko Kuriga nchini Nigeria, Machi 9, 2024. Picha ya AP

Watu wenye silaha nchini Nigeria waliteka nyara watu 61 katika kijiji kimoja katika jimbo la kaskazini la Kaduna, siku chache baada ya wanafunzi 300 kutoweka katika shambulio la genge lenye silaha, wakazi walisema Jumanne.

Makundi yenye silaha, yanayojulikana kama majambazi, yamesababisha uharibifu kwa miaka kadhaa kaskazini mwa Nigeria ambapo yanalenga wanavijiji, madereva wa magari kwenye barabara kuu na wanafunzi ili kupata fidia.

Watu wenye silaha walishambulia jamii ya Buda usiku wa manane siku ya Jumatatu, wakifyatua risasi, mbinu inayotumiwa kutisha, wakazi walisema.

Utekaji nyara mara nyingi hufanyika katika jamii za mbali, na kuwaacha wakazi wakiwa hoi.

Mkazi Lawal Abdullahi alisema hakuwepo wakati watu wenye silaha waliposhambulia lakini mke wake ni miongoni mwa waliotekwa nyara.

“Mke wangu ni miongoni mwa watu 61 waliotekwa nyara na majambazi hao. Bado tunatarajia waombe fidia kama kawaida,” Abdullahi aliiambia Reuters.

Kijiji cha Buda kipo umbali wa kilomita 160 kutoka mji wa Kuriga, ambako wanafunzi walitekwa nyara wiki iliyopita.