Nigeria yaeleza deni lake kwa Shirika la Ndege la Emirates ni takriban $35Million

Ndege ya Shirika la Ndege la Emirates.

Shirika la ndege la Emirates linaidai serikali ya Nigeria kiasi kikubwa cha pesa kutokana na mauzo ya tiketi zake, lakini maendeleo kidogo yamefanyika  ili kuhakikisha kwamba pesa hizo zinalipwa na serikali ya Nigeria.

Waziri wa masuala ya anga nchini Nigeria Hadi Sirika, amewaambia waandishi wa habari kwamba shirika hilo la ndege lenye makao yake huko Dubai, limepokea sehemu kubwa ya pesa hizo, na kwamba karibu dola milioni 35 ndiyo zimebakia.

Shirika la Emirates limekataa kusema kiasi cha pesa ambacho linadai serikali ya Nigeria, lakini msemaji wake amesema kwamba karibu nusu ya kiasi cha pesa ambacho shirika hilo linadai serikali ya Nigeria kimepita muda wake unaostahili kutolewa.

Nigeria inashikilia dola milioni 743 kutoka kwa mashirika ya ndege ya kimataifa yanayofanya shughuli zake nchini humo.