Netanyahu aiita UN "nyumba ya uongo"

Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu

Wakati Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa likijiandaa kukutana kwa dharura Alhamisi ili kutafakari azimio la kupinga Marekani kuitambua Jerusalem kuwa mji mkuu wa Israel, Waziri Mkuu wa Israeli Benjamin Netanyahu ameiita taasisi hiyo ya dunia kuwa “nyumba ya uongo.”

“Taifa la Israeli kwa jumla linatupilia mbali kura hii kabla ya kupigwa,” amesema Netanyahu.

“Jerusalem ni makao makuu yetu na tutaendelea kujenga na kuwepo balozi za nje, zikiongozwa na Marekani, ambayo itahamia Jerusalem.”

Rais wa Marekani Donald Trump aliivunja sera ya muda mrefu ya Marekani mapema mwezi huu akisema kuwa Marekani inaitambua Jerusalem kuwa makao makuu ya Israel na itaanza mchakato wa kuhamisha ubalozi wake huko.

Uamuzi huo wa Marekani umekabiliwa na hatua ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa Jumatatu kufikia azimio linalosema “linasikitishwa sana na uamuzi wa hivi karibuni juu ya kutambuliwa Jerusalem.”

Wanachama 14 wa Baraza hilo kati ya 15 walipiga kura kuunga mkono rasimu ya azimio hilo, lakini Marekani imetumia kura yake ya turufu kulizuia azimio hilo kupitishwa.