Ndege ya South Supreme yaanguka Sudan Kusini, 10 wafariki

Ramani ya Sudan Kusini

Ndege ya shirika la South Supreme imeanguka mara tu baada ya kupaa nchini Sudan Kusini na kuua watu 10 walio kuwemo kwa mujibu taarifa za vyombo vya habari.

Tukio hilo limetokea Jumanne usiku ambapo taarifa za vyombo vya habari zinaeleza kwamba ndege hiyo ilikuwa imebeba abiria wanane, na wafanyakazi wawili.

Ndege hiyo ilikuwa ikielekea katika uwanja wa kimataifa wa Juba, ambapo maafisa wa uwanja wa ndege walithibitisha kutokea kwa ajali hiyo.

Mpaka sasa chanzo cha ajali hiyo hakijaelezwa lakini uchunguzi unaendelea.

Shirika la ndege la South Supreme ni moja ya mashirika muhimu ya ndege nchini Sudan Kusini.

Mwaka 2017 ndege yake moja ilipata ajali nyingine baada ya injini ya ndege kuwaka moto na kuanguka ikiwa safarini kwenda mjini Juba.