Nchi sita zikiwemo Saudia, Misri, UAE zaitenga Qatar kidiplomasia

Mfalme wa Saudi Arabia Salman bin Abdulaziz Al Saud, kushoto, akiongea na Sheikh Mohammed bin Zayed Al Nahyan, Mtawala wa Abu Dhabi na naibu mkuu wa majeshi wa UAE walipokutana Jiddah Saudi Arabia.

Saudi Arabia, Misri, Bahrain, Umoja wa Falme za Kiarabu, Yemen na Maldives wamesitisha mahusiano ya kidiplomasia Jumatatu na nchi ya Qatar, wakiituhumu kuwa inasaidia ugaidi.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Qatar imesema kuwa hatua hiyo “sio ya haki na imejikita katika tuhuma ambazo haziwezi kuthibitishwa na sio za msingi.

Nchi hizo zimesema kuwa zitaondowa maafisa wake wa kidiplomasia kutoka katika nchi yenye utajiri wa gesi na kusitisha safari za anga na baharini kwenda Qatar. Kadhalika shirika la ndege la Qatar limetangaza kusitisha safari zake za ndege kwenda Saudi Arabia.

Misri imempa balozi wa Qatari masaa 48 kuondoka Cairo, wakati nchi za Ghuba ya Uajemi zimetoa kwa raia wa Qatari siku 14 kuondoka katika nchi zao.

Saudi Arabia, ambayo inaongoza umoja wa mataifa yanayopigana kuisaidia serikali ya Yemen, amesema pia vikosi vya Qatar vitaondoshwa kutoka katika mapambano hayo.

Shirika la habari la Serikali ya Saudi Arabia (SPA) limesema Qatar “inavikumbatia vikundi mbalimbali vya kigaidi na vya kikabila vinavyo dhamiria kuharibu utulivu katika eneo hilo, vikiwemo kikundi cha Muslim Brotherhood, Islamic State, na al-Qaida, na mara nyingi imekuwa ikifagilia ujumbe na shughuli za vikundi hivi kupitia vyombo vyake vya habari.

“Qatar imekuwa ikipakwa matope katika kampeni ambayo ni ya uzushi uliokuwa ni uongo mtupu, kitu kinacho thibitisha kwamba kuna mkakati ulioandaliwa makusudi kulichafua taifa hilo,” Waziri wa Mambo ya Nje amesema. Pia amezituhumu nchi hizo kwa kutaka kutafuta sababu ya kuidhibiti Qatar.