Mahakama ya Juu mwezi wa Septemba ilibatilisha ushindi wa Rais Uhuru Kenyatta katika uchaguzi uliofanyika Agosti 8 ukieleza kulikuwa na kasoro za uchaguzi na kuitaka Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kuandaa uchaguzi mpya ifikapo mwisho wa mwezi Octoba.
Kenyatta anatarajiwa kuingia katika kinyang’anyiro hicho mara nyingine akishindana na kiongozi wa Umoja wa Nasa Raila odinga.
Wakili wa mmoja wa wagombea wa urais, James Orengo, alisema Jumatano kwamba iwapo uchaguzi huo hautafanyika katika kipindi kilichowekwa na katiba, basi mamlaka ya Rais wa sasa, Uhuru Kenyatta, yatafikia ukomo.
Lakini akihutubia waandishi wa habari hii leo mjini Nairobi, Mwanasheria Mkuu Githu Muigai amesema kuwa utawala wa sasa utaendelea hadi pale mchakato wa uchaguzi utakamilika na kiongozi atakayechaguliwa kukabidhiwa mamlaka rasmi.
IEBC imetangaza tarehe 26 kuwa siku ya uchaguzi huo, lakini upinzani unataka tume hiyo kufanya marekebisho kadhaa kabla ya zoezi hilo kufanyika.