Maria Sarungi Tsehai kutoka shirika la kutetekea haki za wanawake na mabadiliko ya kisiasa nchini Tanzania amepata umaarufu mkubwa, akiwa na wafuasi milioni 1.3 kwenye mtandao wa X, lakini amelazimika kuishi uhamishoni katika miaka ya hivi karibuni.
Shirika la kutetea haki za binadamu Amnesty International lilitangaza mapema kutekwa kwake Jumapili, likisema “alitekwa nyara na watu watatu waliokuwa na silaha wakiwa ndani ya gari nyeusi aina ya Toyota Noah” katika eneo la Kilimani katikati mwa jiji la Nairobi.
Shirika lake la Change Tanzania, liliandika kwenye mtandao wa X kwamba wanaamini waliomteka nyara “walikuwa maafisa wa usalama wa Tanzania wanaofanya kazi yao nje ya mipaka ya Tanzania ili kuwanyamanzisha wakosoaji”.
Saa kadhaa baadaye, mwenyekiti wa chama cha mawakili wa Kenya Faith Odhiambo aliandika kwenye mtandao wa X kwamba wamefanikiwa kuachiliwa huru kwake.
“Maria Sarungi Tsehai ameachiwa huru na yuko salama kwa sasa,” Odhiambo aliandika.
“Mateso ya kusikitisha aliyokumbana nayo yanatoa taswira ya hali ya wasiwasi ya haki za binadamu katika nchi yetu.”
Alichapisha pia video akiwashukuru wale waliomsaidia akisema “ Leo nimeokolewa.”
Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amekuwa akishtumiwa na makundi ya haki za binadamu na serikali za nchi za Magharibi kwa kusimamia ukandamizaji dhidi ya wapinzani kabla ya uchaguzi ujao mwaka huu, ikiwemo na kukamatwa kwa watu wengi na kutekwa nyara kwa wapinzani.