Abiriga ni mmoja wa wabunge waliokuwa mstari wa mbele kufanikisha marekebisho ya katiba katika kuendeleza utawala wa Museveni. Matamshi ya rais tayari yamezua hasira kutoka kambi ya upinzani.
Akionekana mwenye hasira na kutumia maneno ya matusi kama nguruwe, waoga, wajinga, miongoni mwa mengine, wakati wa mazishi ya Ibrahim Abiriga, mwanasiasa mzalendo wa chama tawala cha NRM, rais wa Uganda Yoweri Museveni amedai kwamba kifo cha mwanasaisa huyo ni cha kisiasa.
Museveni anadai kwamba wanasiasa wa upinzani ndio wahusika wakuu.
Vyama vya Upinzani
Lakini matamshi yake yamewakera wanasiasa wa upinzani wanaomtaka Museveni kuwataja wahusika na kuwakamata, badala ya kutoa madai.
Wanataka ripoti ya mauaji yote ambayo yametokea nchini Uganda yakiwemo ya aliyekuwa msemaji wa polisi Felix Kaweesi, msajili wa mahakama Joan Kagezi, viongozi wa dini ya Kiislamu, watoto, wanawake na utekaji nyara.
Cecilia Ogwal, mbunge wa upinzani, anataka rais Museveni kutaja majina ya wanasiasa wa upinzani anaodai wanahusika na mauaji,pamoja na kuwakamata
Mbunge wa FDC
Mbunge wa Chama cha FDC, Cecilia Ogwal amesema mbona wakuu wa usalama wameshindwa kutambua hao wanasiasa wa upinzani wanaowaua watu kote nchini.
Amesema: “Hili ni dhihirisho kwamba raia hajui kinachoendelea nchini na anafanyia mzaha swala la usalama la nchi hii wakati watu wanaendelea kuawa. Nchi imekuwa kama gari lisilokuwa na dereva wala mwelekezi na linaweza kugonga kitu chochote.”
Kando na kudai kwamba wanasisasa wa upinzani wamemuua mbunge Abiriga, Museveni ametishia kufunga vituo vyote vya habari anavyodai vinatumika na wanasiasa wa upinzani kueneza chuki kuhusu utawala wake akiwataja wahusika kuwa wajinga wanaofanya kelele. Ametishia pia kufunga mitandao ya kijamii anayosema inaeneza porojo.
Amri ya kutofunika kichwa
Amesema kwamba hakuna mtu ataruhusiwa kufunika kichwa wala uso akiwa anaendesha pikipiki. Waendesha piki piki vile vile wanatakiwa kununua kofia mpya zenye namba maalum.
Museveni hakusita kuwalaumu raia kwa kukosa kushirikiana kukabiliana na uhalifu, maafisa wa polisi kwa uzembe, na kusema kwamba kifo cha mbunge Ibrahim Abiriga,aliyemtaja kama mzalendo wake, kimemuuma sana.
Ibrahim Abiriga, alipigwa risasi na watu waliotumia usafiri wa pikipiki. watu kadhaa wameuawa nchini Uganda, vifo ambavyo vimekuwa vikihusishwa na kundi la waasi la Allied democratic forces ADF.