Waziri wa fedha wa Marekani Janet Yellen Jumatano alisema ni muhimu sana kwa Marekani kutimiza ahadi zake za kuiunga mkono Ukraine, na kwamba kutofanya hivyo kutampa nguvu Rais wa Russia Vladimir Putin na wengine kushambulia nchi nyingine za kidemokrasia bila sababu.
Yellen akizungumza na waandishi wa habari wakati wa ziara yake katika mji wa Detroit kunadi maafanikio ya kiuchumi ya utawala wa Biden, alikosoa matamshi ya Rais wa zamani Donald Trump mwishoni mwa Juma, ambapo alidokeza kuwa Marekani haitaendelea kusaidia washirika wake wa NATO ikiwa watashambuliwa.
“Ninayachukulia matamshi hayo kuwa ya kipuuzi sana,” Yellen alisema, akiongeza kuwa alizungumza na maafisa wa kigeni katika siku za hivi karibuni na walielewa kwamba Rais Joe Biden na kundi la wabunge wa Republican na Wademocrat wanaunga mkono NATO na Ukraine.