Mpinzani aliyekamatwa kwa tuhuma za kumtusi Rais wa Algeria aachiliwa

Rais wa Algeria Abdelmadjid Tebboune

Mahakama moja nchini Algeria Alhamisi ilimuachilia mpinzani mashuhuri Fethi Ghares na mke wake chini ya ufuatiliaji wa mahakama wakati uchunguzi kuhusu madai ya kumtusi Rais Abdelmadjid Tebboune na kuhusu mashtaka mengine ukiendelea, wakili wake alisema.

Ghares, mpinzani wa siasa za mrengo wa kushoto, alishtakiwa kwa “kumtusi Rais wa Jamhuri” na “kusambaza taarifa za uongo na matumshi ya chuki kupitia ujumbe kwenye mitandao ya kijamii”, wakili wake, Abdelghani Badi aliiambia AFP.

Messaouda Cheballah, mke wa Ghares, ambaye pia ni mwanaharakati wa kisiasa, alishtakiwa kwa “kuhusika” katika madai ya makosa ya mshtakiwa mkuu, Badi aliongeza.

Wanandoa hao wanatakiwa “kuripoti mahakamani kila baada ya siku 15” wakisubiri tarehe ya kusikilizwa kwa kesi hiyo.

Wamepigwa pia marufuku kutuma habari kwenye mitandao ya kijamii au kuzungumza na vyombo vya habari kabla ya uchaguzi wa Septemba 7, alisema wakili huyo.

Fethi Ghares alikamatwa siku ya Jumanne na polisi nyumbani kwake katika mji mkuu Algiers.