Moto waleta taharuki Dar es Salaam

Ramani ya Tanzania

Moto uliozuka baada ya kupasuka bomba la gesi eneo la kitongoji cha Buguruni Jijini Dar es Salaam umejeruhi watu kadhaa na kuteketeza nyumba katika eneo hilo.

Moto huo ulitokea Jumatatu usiku na kusababisha taharuki kubwa kwa wakazi wa eneo hilo la Mnyamani katika kitongoji hicho.

Mashuhuda wa ajali hiyo wamesema moto huo ulisababishwa na mafundi wa kampuni ya maji safi Dar es Salaam (DAWASCO) waliokuwa kwenye matengenezo ya miundombinu ya maji, ambapo walipasua bomba hilo la gesi.

Vyanzo vya habari nchini Tanzania vimeripoti pia kuwa watu wengi walikimbia makazi yao kwa hofu ya moto huo kusambaa.

Naye Francis Lupokela Afisa mahusiano wa shirika la Petroli Tanzania (TPDC), amesema hivi sasa wanashirikiana na wamiliki wa bomba hilo la gesi kuhakikisha usalama na pia viwanda vilivyoathirika na ukosefu wa gesi kutokana na ajali hiyo na kuhakikisha viwanda hivyo vitaanza uzalishaji.

Mkuu wa Wilaya ya Ilala Sophia Mjema amesema amezungumzia hatua zinazochukuliwa kuhakikisha eneo hilo linakuwa linarejea kuwa salama baada ya mlipuko huo.