Mmiliki wa Telegram afunguliwa rasmi uchunguzi juu ya uhalifu wa mtandaoni

Mwanzilishi wa mtandao wa Telegram Pavel Durov

Jaji mmoja wa Ufaransa Jumatano alimuweka mmliki wa mtandao wa Telegram Pavel Durov chini ya uchunguzi rasmi dhidi ya uhalifu uliopangwa kwenye app hiyo ya kutuma ujumbe.

Jaji huyo alimpa dhamana mjasiriamali huyo kwa sharti la kulipa euro milioni 5, na kuripoti polisi mara mbili kwa wiki na kutuondoka nchini Ufaransa.

Mwendesha mashtaka Laure Beccuau alisema katika taarifa kwamba jaji aligundua kuna sababu za msingi za kufungua uchunguzi rasmi dhidi ya Durov kuhusu mashtaka yote yanayomkabili alipokamatwa siku nne zilizopita.

Mashtaka hayo yanajumuisha tuhuma kwa kusimamia jukwaa la mtandaoni linaloruhusu miamala haramu, picha za udhalilishaji wa kingono dhidi ya watoto, ulanguzi wa dawa za kulevya na ulaghai, pamoja na kupinga kutoa taarifa kwa mamlaka, utakatishaji fedha na kutoa huduma za siri kwa wahalifu.