Mkataba wa amani kati ya Ethiopia na Tigray watimiza miezi sita

Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed

Ethiopia inafikisha miezi sita tangu makubaliano ya kihistoria ya amani kufikiwa.

Chini ya makubaliano hayo ya kihistoria ambayo yalimaliza mzozo wa kikatili wa miaka miwili katika taifa hilo la Afrika Mashariki, TPLF ilikubali kuweka silaha chini kwa mabadilishano kwa Tigray kuweza kufikiwa, ambayo kwa kiasi kikubwa ilitengwa na dunia wakati wa vita.

Vita vilizuka kaskazini mwa Ethiopia zaidi ya miaka miwili iliyopita pale waziri mkuu Abiy Ahmed alipoamuru mashambulizi ya kijeshi dhidi ya chama tawala kilichoasi katika mkoa wa Tigray nchini humo.

Washington imesema kiasi cha watu nusu milioni wamefariki katika mapigano hayo wakati Olusegun Obasanjo, mjumbe wa Umoja wa Afrika katika kanda hiyo akisema huenda wakafikia laki sita.

Novemba mbili pande zilizokuwa zinazozana zilikubaliana kuacha uhasama na Umoja wa Afrika ulipongeza mpango huo kama mwanzo mpya kwa Ethiopia.

Mawasiliano , huduma za benki na umeme vilirejeshwa taratibu katika mkoa huo na kumekuwa na baadhi ya misaada ilirejeshwa.