Kwa mujibu wa shirika la habari la AP, eneo hilo la Mai Tsebri lililoko kaskazini magharibi mwa Tigray liko karibu na mpaka wa kieneo wa Amhara, na limebadilishana mikono mara kadhaa wakati wa vita vilivyoanza 2020 na kumalizika kwa mkataba wa kusitisha mapigano Novemba mwaka jana. Watu wa Amhara wanadai kumiliki eneo hilo.
Tangu Machi mwaka huu, takriban watu 47,000 wamefurushwa kutoka katika eneo hilo la Mai Tsebri wakielekea kwenye mji wa Endabaguna takriban kilomita 55 upande wa kaskazini, kulingana na takwimu za Umoja wa Mataifa, ambazo AP ilizona.Ripoti nyingine iliyotayarishwa na shirika la kibinadamu inasema kwamba wakazi wa Mai Tsebri wamekimbia kutokana na ubaguzi wa kikabila, pamoja na tishio la moja kwa moja kutoka kwa vikosi vya Amhara ambavyo vimekuwa vikiwafukuza.
Ripoti zimeongeza kusema kwamba hakuna misaada ya kibinadamu inayofika kwenye mji wa Endabaguna tangu watu waliotoroka makwao walipoanza kuwasili. Wahamiaji hao wanasemekana kuchukua hifadhi kwenye kituo kilichojengwa na UN pamoja na serikali ya Ethiopia kwa ajili ya wakimbizi kutoka Eritrea, ambayo inapakana na Tigray. Kituo hicho hata hivyo kiliharibiwa vibaya wakati wa mapigano.