Misri na IMF wakubaliana kuongeza mkopo wa dola bilioni nane

  • VOA News

Benki kuu ya Misri iliyoko katika mji mkuu mpya wa utawala, kilomita 45 Mashariki mwa Cairo. Picha na Khaled DESOUKI / AFP.

Misri imesema Jumatano kuwa imefikia makubaliano na Shirika la Kimataifa la Fedha (IMF) kuongeza mkopo wa hadi kufikia dola bilioni nane.

Waziri Mkuu Moustafa Madbouly ametangaza habari hiyo katika maoni yaliyorushwa kwenye television siku ya Jumatano. Kwa miezi kadhaa Misri imekuwa ikifanya mashauriano na IMF kuongeza mkopo wa dola bilioni tatu ambao pande zote zilikubaliana mwaka 2022.

Madbouly amesema makubaliano mapya yataiwezesha serikali kupokea mikopo kutoka taasisi nyingine za fedha, ikiwemo Benki ya Dunia.

Tangazo hilo limekuja saa chache baada ya Benki Kuu ya Misri kuongeza kupandisha kiwango cha riba na kuiweka sarafu yake kwenye soko.

Hatua hiyo imekuwa ni moja ya matakwa ya IMF.

Maana yake ni kupambana na wimbi la mfumuko wa bei na kuvutia uwekezaji wa nje wakati nchi ikikabiliwa na uhaba mkubwa wa fedha za kigeni.

Kufuatia tangazo la sarafu, paundi imeanza kuonyesha mabadiliko ya thamani yake na ndani ya saa kadhaa imeshuka thamani zaidi ya asilimia 60 dhidi ya dola. Ilipofika mapema mchana, benki za biashara zikaanza kufanya biashara kwa dola ya Marekani kwa zaidi ya paundi 50 kwa dola moja, kutoka paundi 31 kwa dola.