Miili 14 ya wanajeshi wa Tanzania yawasili Dar es Salaam

Miili ya wanajeshi wa Tanzania

MIILI 14 ya askari wa jeshi la wananchi wa Tanzania, JWTZ waliouwawa na waasi katika kikosi cha kulinda amani cha UN nchini Jamhuri ya Demokrasia ya Congo (DRC) imewasili leo jijini Dar es Salaam.

Miili hiyo ilipokelewa katika uwanja wa ndege wa jeshi la anga Ukonga jijini Dar es salaam na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Dkt Hussein Mwinyi.

Pia Mkuu wa jeshi la Tanzania, Jenerali Venance Mabeyo pamoja na askari walikuwepo katika mapokezi hayo.

Jeshi limeeleza kuwa miili yote itahifadhiwa katika hospitali ya jeshi ya Lugalo jijijni Dar es Salaam wakati taratibu za kuwaaga zinafanyika

Akizungumza na waandishi katika viwanja hivyo Jenerali Mabeyo alisema shambulio dhidi ya askari hao wa JWTZ katika ulinzi wa amani DRC lilikuwa la kushtukiza lakini halitakwamisha wala kufifisha juhudi za Tanznaia katika kulinda amani.

Jenerali Mabeyo pia amesema askari wengine waliojeruhiwa katika shambulio hilo wamepelekwa maeneo mbalimbali ndani ya DRC na pia nchini Uganda kwa ajili ya matibabu na kwamba hali zao zinaendelea vizuri.

Kwa upande wake waziri wa ulinzi Dk Mwinyi amesema wataendelea kuchukua tahadhari katika maeneo mbalimbali wanayolinda amani duniani ili kuona maafa kama haya hayatokei mara kwa mara.

Askari hao walivamiwa kambini na kundi la waasi wa ADF katika mapigano yaliyodumu kwa takribani saa 13 ambapo askari 14 wa Tanzania waliuwawa, 44 walijeruhiwa na wawili hawajulikani walipo mpaka sasa katika shambulio lililotokea desemba 7 katika kambi ndogo iliyopo kwenye daraja la mto Simulike kaskazini mashariki ya wilaya ya Beni jimbo la Kivu Kaskazini.