Mgogoro wa Sudan: Milipuko na milio ya risasi yatikisa Khartoum na Omdurman

Mkuu wa jeshi la Sudan Jenerali Abdel Fattah Burhan na Jenerali Mohammed Hamdan Dagalo.BURHAN-DAGLO

Milipuko mikubwa na milio ya risasi ilitikisa sehemu za mji mkuu wa Sudan, Khartoum na mji pacha wa Omdurman mapema ijumaa, wakaazi wamesema.

Hili linajiri licha ya kuongezwa muda wa sitisho tete la mapigano kati ya majenerali wakuu wawili ambao mzozo wao wa kugombea madaraka umeuwa mamia ya watu.

Kuongezeka kwa ghasia kulikuja saa chache baada ya pande zote mbili kukubali kuongeza saa 72 za sitisho la mapigano kwa ajili ya kutoa nafasi kwa serikali za kigeni kukamilisha kuwahamisha raia wake kutoka taifa hilo lililokumbwa na machafuko.

Makubaliano ya awali ya muda mfupi hayakuweza kusitisha mapigano, lakini yalipelekea utulivu wa kutosha kwa maelfu ya Wasudan kukimbilia maeneo salama na mataifa jirani kuhamisha raia wake kwa njia ya barabara, anga na bahari.

Mpaka hivi leo makubaliano hayo bado yanaonekana ni magumu.

Mzozo wa kugombea madaraka baina ya jenerali wa jeshi Abdel Fattah Burhan na kiongozi wa wanamgambo jenerali Mohammed Hamdan Dagalo umeharibu matumaini ya kipindi cha mpito nchini Sudan.

Viongozi hao mahasimu waliingia madarakani baada ya kutimuliwa kiongozi mwenye nguvu Omar Al Bashir April mwaka 2019.

Wakati huohuo Sudan inakabiliwa na hatari maradufu ya umaskini na vurugu wakati mapigano yakioendelea.

Pia Umoja wa Afrika umekataa uingiliaji kati wa aina yoyote na wahusika wa nje alisema afisa kutoka AU katika mkutano na waandishi wa habari Jumatano.

Bankole Adeoye, kamishna wa masuala ya siasa , amani na usalama wa tume ya AU amesema kwamba uharibifu mkubwa umefanyika katika miundombinu muhimu ya kitaifa kama vile maji na umeme mjini khartoum na katika miji mingine mingi.

Bankole Adeoye

Adeoye amesema mzozo huo umeitumbukiza Sudan ambayo tayari ni masikini katika hali ya machafuko ambayo hayajawahi kutarajiwa na kusababisha athari zinazoweza kushindwa kurekebishwa katika nchi nzima.

Anasema AU inajitahidi kuzileta pande zote pamoja katika upatanishi na majadiliano.

Kamishna Bankole Adeoye.: “ Uchumi wa Sudan tayari ulikuwa katika hali mbaya kabla ya mzozo. Kwa hiyo tunazungumzia kuhusu Sudan nzima, watu wa Sudan kukabiliwa na mgogoro juu ya mgogoro. Unachoweza kusema ni hatari maradufu.”