Mazungumzo ya moja kwa moja kati ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na waasi wa M23 yataanza katika mji mkuu wa Angola tarehe 18 Machi, ofisi ya rais wa Angola ilisema Jumatano katika taarifa.
Taifa hilo la kusini mwa Afrika limekuwa likijaribu kuwa mpatanishi ili kufikia sitisho la mapigano la kudumu na kupunguza mvutano kati ya Congo na jirani yake Rwanda, ambayo imekuwa ikituhumiwa kuwaunga mkono M23.
Rwanda inakanusha madai hayo.
Angola ilitangaza Jumanne kwamba itajaribu kuanzisha mazungumzo ya moja kwa moja.
Serikali ya Congo ilikataa mara kadhaa kufanya mazungumzo na M23 na Jumanne ilisema imezingatia mpango huo wa Angola.
Hapakuwa maelezo ya mara moja kutoka Kinshasa Jumatano.