Mazungmzo ya kutatua mzozo wa bandari kati ya Ethiopia na Somalia kufanyika Uturuki

Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan. AP Machi 8, 2024

Wakati mazungumzo muhimu ya Somalia yakipangwa kuanza Jumatatu mjini Ankara, Uturuki, waziri mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed amesema kuwa wanatafuta jinsi ya kufikia bandari  kwa njia ya mashauriano.

Kufuatia mawasiliano ya simu na rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan, ambaye taifa lake linaongoza kwenye mashauriano kati ya Somalia na Ethiopia kuhusu utumizi wa bandari, Abiy Ahmed amesema kuwa anakaribisha juhudi za kiongozi huyo.

Ofisi ya Edorgan pia imedhibitisha kuhusu mawasiliano kati ya viongozi hao ambayo pia yameangazia ushirikiano wa kieneo, pamoja na masuala mengine ya kimataifa. Edorgan aliashiria kwamba angependa kuona hakikisho la Ethiopia la kuheshimu utaifa wa Somalia, pamoja na hadhi ya kieneo.