Watu wengine wameripotiwa kuwa walikita kambi sehemu iliyowekwa msiba huo.
Etienne Tshisekedi ameenziwa kitaifa Jumamosi na maziko yake yamehudhuriwa na viongozi wa Afrika wakiwemo marais wa Rwanda na Angola.
Mazishi ya Tshisekedi yamepangwa kufanyika katika kitongoji chake cha Nsele kilomita 40 mashariki mwa Mji mkuu wa Kinshasa.
Mwanasiasa huyo mkongwe alifariki akiwa na umri wa miaka 84 mjini Brussels na mwili wake ulihifadhiwa katika nyumba ya maiti nchini humo hadi wiki iliyopita uliporejeshwa nyumbani DRC.
Ibada maalum ya kumuenzi na kumuombea mwanasiasa huyo maarufu ilifanyika viwanja vya mashahidi mjini Kinshasa wakiongozwa na Askofu Fridolin Ambongo.
Vyanzo vya habari nchini DRC vimeripoti kuwa Kanisa Katoliki lenye nafasi ya kipekee ya ushawishi katika masuala ya kisiasa lilitoa wito kwa wafuasi wake kujitokeza kwa wingi kwenye maziko ya Tshisekedi.
Marais wa Rwanda na Angola walikuwa miongoni mwa idadi kubwa ya watu waliojitokeza kutoa heshima zao za mwisho katika maombolezi hayo.
Imetayarishwa na mwandishi wetu, Washington, DC.