Kikundi cha Wademokrati maarufu, wakiwemo waliokuwa mawaziri wa mambo ya nje John Kerry na Madeleine Albright, wameitaka mahakama iendelee kuzuia amri ya kukataza Waislamu kuingia nchini Jumatatu, wakidai kuwa ilikuwa imetayarishwa vibaya, imetekelezwa ovyo na haikuelezewa vizuri.
"Tunaiona hii amri kama kwamba mwisho wa yote itadhuru usalama wa taifa la Marekani kuliko kulifanya taifa liwe salama," wamesema, kinyume na maelezo ya Trump kwamba amri ya kukataza wahamiaji itaimarisha usalama wa taifa.
Makampuni mengine 97, ikiwemo Silicon Valley, Giants Apple, Facebook, Google, Microsoft na Twitter, wamefungua kesi Jumapili jioni katika mahakama hiyo, wakiunga mkono kesi ya kupinga amri ya kuzuia kusafiri.
Wiki iliyopita, Jaji wa Mahakama ya Wilaya Marekani James Robart wa Jimbo la Washington alizuia kwa muda amri ya kiutendaji ya muda ya Trump ilioleta usumbufu kwa wasafiri wakimbizi waliokuwa wakija Marekani na wahamiaji wengine kutoka nchi saba zenye waislamu walio wengi: Iran, Iraq, Libya, Somalia, Sudan, Syria na Yemen.
Siku ya Jumapili, mahakama ya rufaa ilitupilia mbali matakwa ya uongozi wa Trump kutaka amri hiyo irudishwe kuzuia wasafiri.