Mashambulizi hayo yalifanyika saa chache baada ya Rais Felix Tshisekedi kutangaza hali ya tahadhari na kuzingirwa kwa majimbo mawili, na maafisa wa usalama.
Kuongezeka kwa mashambulio ya wanamgambo wenye silaha na vurugu mashariki mwa DRC kumepelekea mauaji ya zaidi ya watu 300 tangu mwanzo wa mwaka 2021, wakati wanajeshi wa serikali na walinda amani wa Umoja wa Mataifa wakijitahidi kutuliza hali hiyo.
Mashambulio ya hivi karibuni yalitokea mapema Jumamosi wakati wanamgambo walipovamia vijiji viwili katika mji wa Beni, jimbo la Kivu Kaskazini, viongozi wa eneo hilo walisema.
Baadaye siku hiyo, mmoja wa maimamu wenye ushawishi mkubwa mjini humo, alipigwa risasi na kuuawa na washambuliaji wasiojulikana ndani ya msikiti mkuu wa Beni, wakati wa sala ya jioni, kulingana na ripoti za vyombo vya habari.
Tshisekedi alikuwa ametangaza hali ya tahadhari, katika majimbo ya Kivu Kaskazini na Ituri Ijumaa.
"Lengo ni kumaliza haraka ukosefu wa usalama ambao unaua raia wenzetu katika sehemu hiyo ya nchi kila siku," msemaji wa serikali Patrick Muyaya alisema.
Hakusema ni hatua gani zitachukuliwa baada ya mashambulizi hayo. Kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters, Kikundi cha waasi cha Uganda kilichokita kambi mashariki mwa Kongo tangu miaka ya tisini, kiitwacho ADF, kinashutumiwa kutekeleza mauaji mengi, katika siku za karibuni.