Uongozi wa Trump wapitisha masharti makali zaidi ya kutoa viza

Rais Donald Trump

Uongozi wa Trump umeanzisha aina mpya ya maswali yenye masharti makali zaidi kwa wale wanaoomba viza duniani kote kuja Marekani.

Utaratibu huo unataka muombaji aonyeshe mawasiliano yake ya mitandao ya jamii ya miaka mitano na taarifa za maisha yake za miaka kumi na tano iliyopita.

Maswali hayo mapya, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuwachunguza wale wanaotaka kutembelea Marekani, yamepitishwa Mei 23 na Ofisi ya Utawala na Bajeti.

Hata hivyo pamekuwapo ukosoaji wa utaratibu huo kutoka kwa maafisa kadhaa wa elimu na makundi ya wanazuoni katika kipindi ambacho watu walikuwa wanatoa maoni yao kuhusu utaratibu huu.

Wanaokosoa utaratibu huu wanadai kuwa maswali mapya yatakuwa ni mzigo mkubwa, na kupelekea ucheleweshaji wa utayarishaji wa visa na pia kuwavunja moyo wanafunzi wa kimataifa na wanasayansi kuja Marekani.

Chini ya utaratibu mpya, maafisa wa ofisi za visa wanaweza kuomba namba za zamani za pasi ya kusafiria, taarifa za mawasiliano ya mitandao za miaka mitano, anuani za barua pepe na number za simu na taarifa za maisha ya wanaombaji visa za miaka 15, ajira na sehemu walizo safiri. (bit.ly/2qBSrpv)

Maafisa wataomba taarifa za ziada iwapo wataona kuwa “taarifa hizo zinahitajika kuthibitisha utambulisho au tabia za undani katika uchunguzi wa usalama wa taifa,” afisa wa Wizara ya Mambo ya Nje amesema Jumatano.

Wizara ya Mambo ya Nje imesema mapema uchunguzi wa kina utawagusa wale wanaoomba visa “ambao imethibitika kuwa wanahitaji uchunguzi wa ziada kuhusiana na vitendo vya ugaidi au masuala mengine ya kiusalama ambayo yanazuilia kupewa visa.”