Mashambulizi ya Israel huko Gaza yameua watu 20 Jumamosi, maafisa wa afya wamesema, huku Qatar ikielezea matumaini ya kasi mpya katika juhudi za kufikia makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya Israel na Hamas.
Jeshi la Israel halikutoa maelezo mara moja juu ya mashambulizi hayo yaliyoripotiwa katika mji wa Gaza wa Rafah.
Wanane kati ya waliouawa walikuwa raia, kulingana na wakazi na madaktari. Haikufahamika wazi ikiwa wengine waliouawa walikuwa wapiganaji.
Waziri mkuu wa Qatar ambaye pia ni waziri wa mambo ya nje Sheikh Mohammed bin Abdulrahman Al Thani amesema Qatar imeanzisha mazungumzo na utawala ujao wa Trump kuhusu Gaza baada ya matumaini chanya ya kufufua mazungumzo ya sitisho la mapigano kufuatia uchaguzi wa Marekani.