Sweden iliishinda Marekani kwa mabao 5-4 na kufuzu kuingia kwenye robo fainali na kumzuia bingwa huyo wa mara mbili kutwaa mataji matatu ya kihistoria mfululizo.
Mechi hiyo iliyofanyika mjini Melbourne, Australia, iliamuliwa kwa njia ya video (VAR), huku mwamuzi Stephanie Frappart - baada ya kukagua yaliyojiri- akiona kuwa penalti ya Lina Hurtig ilivuka mstari licha ya Mlinda lango wa timu ya Marekani Alyssa Naeher kugusa mpira huo, na kuonekana kama angeokoa timu yake.
Wachezaji wa Sweden walisherehekea kwa furaha, huku kukiwa na vilio kutoka kwa timu ya Marekani, ushiriki wake ukiisha katika hatua ya 16 bora, ikiwa ni mara ya kwanza kabisa Marekani kuwahi kuondoka kwenye Kombe la Dunia la Wanawake.
Huku kukiwa hakuna bao baada ya dakika 120 za mchezo - dakika 90 za muda wa kawaida na dakika 30 za muda wa ziada - mechi ilibidi kuamuliwa kwa mikwaju ya penalti.
Nathalie Bjorn wa Sweden alikuwa mchezaji wa kwanza kukosa nafasi hiyo, na kumpa Megan Rapinoe, ambaye kwa sasa ameichezea nchi yake mechi yake ya mwisho ya michuano mikubwa, nafasi ya kuiweka Marekani mbele kwenye mikwaju ya penalti na bado Rapinoe – ambaye kwa kawaida ndiye anayetegemewa zaidi kati ya wapiga penalti – alikosa, na kuipatia Sweden matumaini tena.