Trump amesema hayo Ijumaa wakati akihutubia wafanyakazi wa jeshi na familia zao katika kambi ya Andrews huko Maryland, nje kidogo ya jiji la Washington.
Amesema kitendo cha Korea Kaskazini cha kufyetua kombora saa chache ziliyopita wakati akizungumza inaonyesha jinsi gani Pyongyang inavyowadharau majirani zake na jumuiya ya kimataifa kwa ujumla.”
Mapema siku ya Ijumaa, Ushirika wa NATO ulitaka kuwe na hatua za pamoja dunia nzima kukabiliana na kufyetuliwa kwa kombora hilo, ambalo lilipita katika anga ya Japan siku chache baada ya Umoja wa Mataifa kuweka vikwazo vipya dhidi ya Pyongyang kwa kufanya jaribio la sita la nyuklia.
Katibu Mkuu wa Nato Jens Stoltenberg amesema katika ujumbe wa Twitter, “ kitendo cha Korea Kaskazini kurusha kombora ni uvunjifu mwengine wa azimio la Umoja wa Mataifa – ambalo ni tishio kubwa kwa amani na usalama wa kimataifa ambalo linahitaji hatua za pamoja zikijumuisha mataifa yote."
Huko Umoja wa Mataifa, Baraza la Usalama lilikutana kwa faragha kwa zaidi ya saa moja.