Takriban watu 30 wanahofiwa kufariki baada ya maporomoko ya ardhi katika kijiji kimoja mashariki mwa Uganda, afisa mmoja wa eneo hilo alisema siku ya Alhamisi, akionya kwamba huenda idadi hiyo ikaongezeka.
Nchi hiyo ya Afrika Mashariki imekumbwa na mafuriko na mvua kubwa katika siku chache zilizopita, huku serikali ikitoa tahadhari ya maafa baada ya ripoti za mafuriko na maporomoko ya ardhi.
Kijiji cha Masugu mashariki mwa wilaya ya Bulambuli, ambacho ni umbali wa saa tano kutoka mji mkuu, Kampala, kilikumbwa na maporomoko ya udongo Jumatano jioni.
Picha kwenye vyombo vya habari vya ndani zilionyesha maporomoko makubwa huku wanafamilia wakiomboleza, na wengine kuelezea masikitiko yao. "Tulipoteza takriban watu 30," mkuu wa wilaya Faheera Mpalanyi aliambia AFP. Aliongeza kuwa miili sita, ikiwa ni pamoja na wa mtoto, imepatikana hadi sasa.