Wanawake wanne na mtoto moja wamepoteza maisha baada ya maporomoko ya matope kufunika nyumba zao kufuatia mvua kubwa eneo la Bukavu huko mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), shirika la habari la AFP limeripoti Jumamosi.
“Miili mitano imepatikana katika eneo la pamoja watu wanakoishi huko Kadutu baada ya maporomoko hayo kufuatia mvua kubwa” usiku kucha, mwakilishi wa serikali ya mtaa Hypocrate Marume amesema.
Amesema waliopoteza maisha ni wanawake wanne na mtoto moja wa kiume – idadi inayolingana na ile iliyotolewa na meya Munyole Kashama – akiongeza juhudi ya kuitafuta miili mingine iliyofunikwa katika maporomoko hayo zinaendelea.
Kashama ameongeza kuwa siyo chini ya watu wanne walikuwa wamejeruhiwa.
Mwaka 2017 maporomoko yalisababisha vifo vya watu 40 katika Kijiji cha uvuvi kilichoko mkoa wa kaskazini mashariki mwa Ituri.