Mapigano makali yaua watu 65 nchini Sudan

Ramani ya Sudan

Ramani ya Sudan

Mapigano makali huko kusini na magharibi mwa Sudan yaliua watu 65 na kujeruhi wengine zaidi ya 130 Jumatatu, madaktari wamesema, huku vita vibaya kati ta jeshi na kundi la wanamgambo vikipamba moto tena.

Huko Kordofan Kusini, shambulizi la mizinga kwenye mji mkuu wa jimbo hilo wa Kaduguli liliua watu 40 na kujeruhi wengine 70, kulingana na vyanzo viwili vya madaktari.

Mji huo unaodhibitiwa na jeshi la Sudan, ulilengwa katika shambulizi ambalo Gavana wa jimbo Mohamed Ibrahim anasema lilitekelezwa na tawi la kundi la waasi la The Sudan People’s Liberation Movement -North au SPLM-N linaloongozwa na Aziz al-Hilu, ambalo pia lina ngome zake katika jimbo hilo.

“Shambulizi la Hilu dhidi ya raia ndani ya Kaduguli lina lengo la kuyumbisha” usalama wa eneo hilo, Ibrahim alisema katika taarifa iliyotumwa kwa AFP, akiapa “kuwafurusha waasi kwenye milima karibu na Kaduguli”.

Gavana huyo alisema shambulizi hilo lililenga soko moja.

SPLM-N ilipigana na jeshi pamoja na wanamgambo wa kikosi cha Rapid Support Forces (RSF) katika maneo tofauti ya Kordofan Kusini katika vita vyao.

Sudan imekumbwa na mzozo tangu mwezi Aprili 2023, huku mapigano kati ya jeshi la serikali na kikosi cha RSF yakipamba moto katika wiki za hivi karibuni.

Katika jimbo kubwa la Darfur, shambulizi la anga la jeshi kwenye mji mkuu wa Darfur Kusini, Nyala, liliua watu 25 na kujeruhi wengine 63 Jumatatu, chanzo cha madkatari kimeiambia AFP.