Wanafunzi wa Lucky Vincent warejea shuleni

Wanafunzi wa Lucky Vincent wakiwa na wazazi wao baada ya kuwasili kutoka Marekani walipokuwa wanapatiwa matibabu.

WANAFUNZI watatu wa Shule ya Lucky Vincent, Wilaya ya Karatu, jijini Arusha wamehudhuria masomo yao darasani Jumatano kwa mara nyingine huku wanafunzi wenzao wakifurahia uwepo wao shuleni.

Wanafunzi hao Sadya Awadhi, Wilson Tarimo na Doreen Elibariki, waliwasili kwa usafiri wa pamoja binafsi shuleni eneo la Kwa Mrombo huku wakisindikizwa na wazazi wao.

Wiki mbili zilizopita manusura hawa wa ajali ya gari ya shule ya Lucky Vincent iliyotokea katika eneo la Rhotia mnamo tarehe 6 mwezi mei walirejea nchini Tanzania kutoka Marekani walikokuwa wakipatiwa matibabu kwa Zaidi ya miezi mitatu.

Kwa mujibu wa gazeti la Habari Leo Mwalimu Mkuu Msaidizi wa Lucky Vincent, Longino Mkama, watoto hao waliwasili jana asubuhi, na walipofika walipokelewa na wanafunzi wenzao huku kila mmoja akishangilia hususan wanafunzi wa darasa la saba, waliokuwa wakisoma nao kabla ya kupata ajali iliyosababisha wapelekwe Marekani kwa matibabu zaidi.

“Ukweli tumejisikia faraja kuwaona watoto hawa wakiwa darasani wakihudhuria masomo yao na wenzao na hawaoneshi tofauti yoyote na sisi tumewapokea na wanaendelea na masomo yao hadi watakapofanya mitihani yao,” alieleza Mwalimu Mkama.

Juzi wazazi wa watoto hao walimuomba Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo kuwasaidia ili watoto wafanye mtihani wa kumaliza darasa la saba mwaka huu. Aidha, Gambo alikabidhi Sh 23,273,885 kwa wazazi watatu ambapo kila familia ilipewa Sh mil. saba.