Manusura katika ajali ya jengo lililoporomoka Afrika Kusini aokolewa baada ya siku tano

Waokoaji wakimbeba manusura katika ajali ya jengo lililoporomoka katika mji wa George nchini Afrika Kusini, Mei 11, 2024.

Waokoaji na wapita njia walishangilia na kupiga makofi Jumamosi wakati manusura mmoja alipookolewa baada ya saa 116 kutoka chini ya vifusi vya jengo lililoporomoka nchini Afrika Kusini, ajali ambayo iliua watu 13.

“Ni muujiza ambao sote tumekuwa tukiutarajia”, mkuu wa jimbo Alan Winde alisema kwenye mtandao wa X.

Jumba la ghorofa lililokuwa likijengwa katika mji wa kusini wa George liliporomoka siku ya Jumatatu alasiri wakati wafanyakazi 81 walikuwa kwenye eneo la ujenzi.

“Tuliposhuka chini ya kifusi ambacho hatukuwa tumekiona, tulisikia mtu ndani na tukasimamisha shughuli zote kubwa,” Colin Deiner, mkuu wa shughuli za uokoaji aliwaambia waandishi wa habari.

Waokoaji walimuita manusura huyo na akajibu, Deiner ameongeza.