Kwa mujibu wa serikali ya Uganda, mali zake Mukulu anayekabiliwa na mashtaka kadhaa ya mauaji, inaaminika kuwa iko mikononi mwa baadhi ya watu nchini Tanzania.
Mwandishi wa idhaa ya Kiswahili VOA anaripoti kuwa miaka miwili baada ya kamanda wa waasi wa ADF Jamil Mukulu kukamatwa nchini Tanzania, serikali ya Uganda imechukua hatua ya kumiliki mali zake zote na kuzuia kusimamia mali hizo yeye mwenyewe au mtu yoyote mwengine.
Kiongozi wa mashtaka ya umma nchini Uganda Mike Chibita, amewaeleza waandishi wa habari baada ya kuhojiwa kwa masaa kadhaa na kamati ya bunge kuhusu sheria, kwamba wawakilishi wa serikali tayari wapo nchini Tanzania, kuhakikisha kwamba mali zote za kiongozi huyo wa waasi, inasimamiwa na serikali.
“Wawakilishi wetu wameenda nchini Tanzania kuorodhesha mali zake mshtakiwa. Sheria inaturuhusu kusimamia mali zake” ameeleza Mike Chibita, msimamizi wa mashtaka ya umma nchini Uganda.
Mukulu alikamatwa nchini Tanzania mnamo April mwaka 2015 baada ya kusakwa kwa muda wa miongo miwili.
ADF ni kundi la waasi kutoka nchini Uganda lenye maficho yake katika Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo, DRC, na Serikali ya Uganda inaamini kwamba Jamil Mukulu, ana biashara kadhaa katika nchi za Kenya na Tanzania, zenye thamani ya mabilioni ya pesa, zinazotumika kufadhili shughuli za kundi hilo, hasa kununua silaha.
Kundi la ADF linashutumiwa kutekeleza mauaji ya watu mashuhuri katika serikali ya Uganda wakiwemo viongozi wa dini ya Kiislamu, na wanajeshi.
Waasi hao wanashutumiwa kumuua aliyekuwa kiongozi wa mashtaka ya ugaidi Joan Kagezi aliyekuwa akisimamia kesi ya mashambulizi ya bomu nchini Uganda. Mukulu, anazuiliwa katika kituo cha polisi cha Nalufenya, mjini Jinja, wanakozuiliwa washukiwa wanaochukuliwa kuwa hatari kwa usalama wa taifa.