Wapiganaji wa kundi la mamluki wa Russia la Wagner ni miongoni mwa waliouawa katika mapigano hayo, ambayo yalifanyika mwishoni mwa mwezi Julai kaskazini mwa nchi.
Mali imevunja uhusiano “ na hatua hiyo imeanza kutekelezwa mara moja”, alisema msemaji wa serikali Kanali Abdoulaye Maiga.
Maiga aliongeza kuwa serikali ya Mali ilikasirishwa na matamshi ya Andriy Yusov, msemaji wa idara ya ujasusi ya Ukraine.
Taarifa ya Maiga iliongeza kuwa Yusov “alikiri kuhusika kwa Ukraine katika shambulizi la kikatili la makundi ya kigaidi yenye silaha” ambalo lilisababisha vifo vya wanajeshi wa Mali.
Kitendo cha Ukraine kilikiuka uhuru wa Mali na ni uingiliaji kati wa kigeni usiokubalika na uungaji mkono wa ufadhili wa ugaidi wa kimataifa, taarifa hiyo ilisema.
Mapigano makali ya siku tatu yalizuka tarehe 25 Julai karibu na mpaka wa Algeria kwenye kambi ya kijeshi katika mji wa Tinzaouatene.
Kundi la waasi wanaotaka kujitenga linaloongozwa na Watuareg Alhamisi lilisema liliua wapiganaji 84 wa Wagner na wanajeshi 47 wa Mali.
Katika video iliyoonwa na shirika la habari la AFP siku ya Ijumaa, waziri mkuu wa Mali Choguel Kokalla Maiga alikiri kwamba walishindwa “katika vita” huko Tinzaouatene.