Malaysia yawafungulia mashtaka raia wanne wa Thailand kuhusiana na miili iliyofukuliwa katika makaburi ya pamoja

Mabaki ya miili ya wanadamu waliokuwa katika makaburi ya pamoja eneo la kambi zilizokuwa zinatumiwa na wasafirishaji haramu wa watu katika msitu ulioko katibu na mpaka wa Thailand, huko Bukit Wang Burma, Malaysia Mei 26, 2015.

Raia wanne wa Thailand walifunguliwa mashtaka Ijumaa chini ya sheria za kupambana na usafirishaji haramu wa watu nchini Malaysia ikiwahusisha na kugunduliwa kwa makaburi kadhaa ya pamoja yanayosadikiwa kuwa waliozikwa humo ni Waislam wa Rohingya na Wabangladeshi.

Watu hao inadaiwa waliokuwa wanashikiliwa katika kambi kadhaa kwenye msitu ulioko mlimani kwenye mpaka wa nchi hiyo na Thailand.

Waziri wa Mambo ya Ndani Saifuddin Nasution alisema katika taarifa yake kuwa wanne hao walikuwa kati ya raia wa Thailand 10 ambao serikali ilitaka wahamishwe kuja Malaysia kujibu mashtaka mwaka 2017 kutokana na janga lililotokea huko Wang Kelian magharibi mwa jimbo la Perlis lililolishitua taifa.

Kufuatia ushirikiano uliotolewa na mamlaka za Thailand, alisema watu hao wanne walikamatwa na kusafirishwa Malaysia Alhamisi kushtakiwa.

Mwezi Mei 2015, polisi nchini Malaysia ilitangaza kugunduliwa kambi zilizokuwa zimetelekezwa katika msitu zilizokuwa zikitumiwa na wasafirishaji haramu wa binadamu huko Wang Kelian na baadaye miili 139 ilifukuliwa kutoka katika makaburi ya pamoja.

Ugunduzi huo unafuatia kama ule wa awali uliogunduliwa na polisi wa Thailand, ambapo miili 36 ilifukuliwa kutoka katika makaburi yenye kina kidogo upande wa mpaka wa Thailand.

Chanzo cha habari hii ni shirika la habari la AP.