Makonda achunguzwa kwa kashfa ya uvamizi wa 'Clouds'

Waziri Nape Nnauye

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Tanzania, Nape Nnauye ameunda Jumatatu timu ya watu watano watakao fanya uchunguzi juu ya madai kuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda alivamia chombo cha habari cha Clouds Media Group.

Waziri Nnauye ameipa timu hiyo masaa 24 kuwasilisha ripoti yao wizarani na kumshauri hatua za kuchukuliwa.

Timu hiyo imetakiwa kwenda kumtafuta Mkuu wa Mkoa na kufanya mahojiano nae ilikupata maelezo ya upande wake kuhusiana na madai haya.

“Kwa kuwa tumepata madai ya upande mmoja, tunataka tupate upande wa Mkuu wa Mkoa na watu wake ili tujue kwa nini wamefanya walichokifanya, kujua maelezo yao ni nini kabla hatujachukua hatua,” amesema waziri huyo.

Wakati watanzania wakisubiri kuona hatua zitakazochukiliwa dhidi ya madai hayo, ya uvamizi wa chombo cha habari, Rais John Magufuli alipokuwa anazindua ujenzi wa barabara ya juu katika makutano ya barabara ya Mandela , Sam Nujoma na Morogoro jijini Jumatatu, alimtaka Mkuu wa Mkoa kuendelea kuchapa kazi, kwa vile yeye kama rais hafanyi kazi kupitia mitandao ya kijamii.

Mkurugenzi wa Maelezo

Waziri Nnauye ameitaja timu hiyo itaongozwa na Mkurugenzi wa Habari Maelezo, Hassan Abbasi, wakiwemo mwakilishi kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), na wengine kutoka katika tasnia ya habari Jesse Kwayo-IPP Media, Balile –gazeti la Jamhuri, na mhariri wa Wapo radio Nengida.

Waziri amesema serikali inalaani kilichotokea kwa nguvu kubwa kama kilichotokea na kilicho elezwa ndicho kilichotokea.

“Serikali kwa nguvu kubwa tunalaani jambo hili, kwa sababu halifai na wala halipaswi kutokea,” amesema Nnauye.

Tanzania inaheshimu uhuru wa habari

Amesisitiza kwamba hili halipaswi kutokea kwenye nchi kama Tanzania ambayo imesaini mikataba mbalimbali ya kimataifa juu ya uhuru wa vyombo vya habari, kwenye nchi ambayo katiba yake na sheria zake zinataka uhuru wa habari ulindwe.

Pia ameongeza kuwa hili halipaswi kutokea kwenye nchi ambayo imekuwa na historia ya kuheshimika na kutukuka duniani kuwa kutoa uhuru kwa vyombo vya habari.

Waziri huyo ameongeza kuwa kitendo hichi kilichofanyika ni kunajisi uhuru wa vyombo vya habari “katika nchi yetu.”

Wakati wa ziara yake katika kituo hicho cha Clouds, amesema “sisi kama serikali tunataka kutoa wito hapa” kwamba wanahabari wasivunjike moyo kwa jambo lililo tokea.

Msimamo wa serikali

“Serikali kwa ujumla wake iko na nyie, na serikali ipo kulinda haki zenu, ili mtimize wajibu wenu vizuri bila ya kuingiliwa, bila ya kushinikizwa, na lolote lililotokea,” waziri amefafanua.

Taarifa za uvamizi wa mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda katika chombo hicho cha habari cha Clouds Ijumaa usiku zilianza kusambaa kwenye mitandao ya kijamii, jana na kulazimu kampuni hiyo inayomiliki redio na televisheni kutoa taarifa rasmi kupitia kwa mkurugenzui wake wa vipindi Ruge Mutahaba, akithibitisha tukio hilo lililozua taharuki katika tasnia ya habari.

Mkuu wa Mkoa

Kwa mujibu wa vyanzo vya habari inadaiwa Mkuu wa Mkoa alikuwa anafuata taarifa nyeti aliyowakabidhi watayarishaji wa kipindi kimoja cha udaku ili wakirushe ikiwa ni vita yake dhidi ya askofu mkuu wa kanisa la ufufuo na uzima, Josephat Gwajima tangu alivyo mtaja katika sakata la dawa za kulevya

Kamati ya Bunge

Mwenyekiti wa Kamati ya bunge ya huduma na maendeleo ya jamii Peter Serukamba amesema jambo hili ni fundisho hasa kwa waandishi wa habari kwamba wasikubali kutumiwa na wanasiasa.

“Hii ni kwa sababu sisi wanasiasa tunakuja kwenye vyombo vya habari, tunatengeneza ujamaa hivyo tunaweza kulazimisha mambo ambayo ni nje ya utaratibu,” amesema Mwenyekiti huyo.

“Nimeona niseme hili kwa waandishi wa habari, kwamba hili tukio liwe fundisho kwenu. Tusikubali kutumika, fanyeni kazi yenu kulingana na weledi wa kazi zenu,” amesisitiza.

Utumiaji mbaya wa madaraka

Mwenyekiti huyo amesema alichofanya mkuu wa mkoa kwa namna yoyote ile ni utumiaji mbaya wa madaraka aliyopewa.

“Sisi kama kamati tunasubiri serikali imechukua utaratibu, imeunda kamati, wakishamaliza ripoti yao wataileta kwetu… Na tutatoa maoni yetu na kushauri baada ya kupata ripoti ya hiyo kamati,” amesema.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa chama cha wamiliki wa vyombo vya habari Reginald Mengi naye amewahamasisha waandishi kwamba tukio hili lisiwaogopeshe wakaacha kufanya kazi zao kama kawaida.

“Lakini mwandishi wa habari jasiri haogopi anafanya kazi yake. Lakini anafanya kihalali na kufuata kanuni ya tasnia hii,” amesema Mengi.