Makamishna 3 wa IEBC wajiuzulu

Mwenyekiti Wafula Chebukati

Makamishna watatu kati ya sita wa Tume ya Uchaguzi nchini Kenya wamejiuzulu wakati ambapo taasisi hiyo inakabiliwa na migogoro.

Kwa mujibu wa vyanzo vya habari nchini Kenya naibu mwenyekiti wa tume hiyo Connie Nkatha Maina, Margaret Mwachanya na Paul Kurgat wametia ila uongozi wa Mwenyekiti Wafula Chebukati akidai kuwa hana uwezo wa kuongoza tume hiyo wakati wakitangaza kujiuzulu kwao Jumatatu.

“Kwa muda mrefu hivi sasa na mara nyingi kabisa, mwenyekiti wa tume hii ameshindwa kuwa imara na kudhibiti katika kuiongoza meli hii katika kipindi kigumu na kutoa maelekezo yanapohitajika,” watatu hao waliojiuzulu wamesema katika tamko lao.

Wameongeza kuwa: “Badala yake chini ya uongozi wa Chebukati, Chumba cha mikutano cha Tume hiyo kimekuwa ni uwanja wa kutoa taarifa za upotoshaji, mahali pakuendeleza kutokuaminiana na sehemu ya kushindana na kufukuzana kutafuta sifa na utukufu binafsi.”

Wakati wakiweka msimamo kuwa hawana imani na Chebukati, walisisitiza kuwa uchaguzi uliobatilishwa Agosti ulikuwa umefanyika kihalali.