Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Desemba 24, 2024 Local time: 20:09

Mwanasiasa maarufu wa Kenya Kenneth Matiba afariki


Mwanasiasa na mwanaharakati wa kutetea demokrasia ya vyama vingi nchini Kenya Kenneth Matiba.
Mwanasiasa na mwanaharakati wa kutetea demokrasia ya vyama vingi nchini Kenya Kenneth Matiba.

Mwanasiasa mkongwe wa Kenya, Kenneth Matiba, ambaye alikuwa mmoja wa wanaharakati wakuu wa kutetea uwepo wa demokrasia ya vyama vingi vya kisiasa nchini humo, aliaga dunia Jumapili usiku akiwa na umri wa miaka 85.

Matiba, ambaye kwa wakati mmoja aliwania urais na kuchukua nafasi ya pili, alifariki katika Hospitali ya Karen jijini Nairobi baada ya kuugua kwa muda mrefu.

Vyombo vya habari nchini Kenya vilinukuu famila yake ikisema kuwa alikufa kutokana na mshtuko moyo ulioifanya damu yake kukosa kusambaa mwilini.

Matiba, ambaye amewahi kutiwa kizuizini kwa sababu za kisiasa atakumbukwa kwa juhudi zake za kupambana na utawala wa chama cha KANU mnamo miaka ya tisini.

Alikuwa mmoja wa wananzilishi wa chama cha upinzani FORD ambacho baadaye kiligawanyika na kuwa vyama kadhaa na pia alihudumu kama waziri katika wizara mbalimbali kabla ya kutangaza azima yake ya kuwania urais.

Akiwa na wenzake, Matiba alikuwa msitari wa mbele kumshinikiza rais wa wakati huo kukubali kuondoa kipengele cha katiba cha 2A, kilichopiga marufuku uwepo wa vyama vingi nchini Kenya.

Mnamo mwaka wa 1992, akiwa na chama cha Ford Asili, alikaribia kumshinda rais wa kipindi hicho Daniel Arap Moi katika uchaguzi ambao wafuasi wake waliutaja kuwa usio wa haki na kweli.

Kiongozi huyo wa zamani wa Upinzani, aidha alikuwa mjasiriamali tajika aliyemiliki migahawa kadhaa ya kifahari kati ya biashara zingine.

Punde baada ya kupata habari za kifo chake, rais Uhuru Kenyatta alilihutubia taifa kupitia vyombo vya habari na kusema kuwa taifa hilo limempoteza mzalendo.

Hata hivyo baadhi ya Wakenya walikosoa tawala ambazo "hazikuwatambua ipasavyo mashujaa wa uhuru wa pili."

Mbunge wa zamani Njeru Kathangu alisema: "Tunayaona machozi ya mamba kutoka kwa wale waliochangia ugonjwa wa Matiba."

Alipokuwa kizuizini wakati wa utawala wa rais Moi, Matiba alipooza upande mmoja wa mwili na hakupona ugonjwa huo hadi kifo chake.

XS
SM
MD
LG