Viongozi wa mataifa wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki watakutana Jumatatu kujadili hali ya usalama katika eneo la mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Afisi ya rais wa Kenya ilimesema Jumapili.
Mkutano huo unajiri wakati mapigano makali yamefufua uhasama wa miongo kadhaa kati ya Kinshasa na Kigali, huku DRC ikiilaumu jirani yake, Rwanda, kwa kuibuka upya hivi karibuni kwa kundi la waasi la M23. Rwanda imekanusha mara kwa mara kuwaunga mkono waasi hao huku nchi zote mbili zikilaumiana kwa kufanya mashambulizi ya kuvuka mpaka.
“Watu mashariki mwa DRC wameteseka kwa muda mrefu na wanaendelea kulipa gharama kubwa kupita kiasi kwa kupoteza maisha, mali na ukosefu wa amani," afisi ya rais wa Kenya ilisema katika taarifa yake ya kutangaza mkutano wa Jumatatu mjini Nairobi. Siku ya Jumatano, Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta alitoa wito wa kutumwa kwa kikosi cha kanda ya Africa mashariki nchini DRC ili kurejesha hali ya amani, lakini Kinshasa ilisema haitakubali ushiriki wa Rwanda katika operesheni hiyo.
Rais wa DRC Felix Tshisekedi ameishutumu Rwanda kwa kutaka "kuchukua ardhi yetu, yenye utajiri wa dhahabu, kobalti na madini mengine, kwa ajili ya kujinufaisha" na kuitaka jumuiya ya kimataifa kulaani Kigali.
Kikosi cha Umoja wa Mataifa kinachojulikana kwa kifupi kama MONUSCO, tayari kipo nchini DRC.