Majaji nchini Afrika Kusini kuamua ikiwa Zuma atagombea kwenye uchaguzi wa Mei 29

Rais wa Zamani wa Afrika Kusini Jacob Zuma

Majaji nchini Afrika Kusini leo Jumanne wataamua ikiwa rais wa zamani Jacob Zuma ataruhusiwa kugombea kwenye uchaguzi wa Mei.

Zuma, ambaye anawania kwa kitiki ya chama cha upinzani, alikata rufaa dhidi ya uamuzi wa maafisa wa tume ya uchaguzi waliomkatalia kugombea kutokana na kupatikana na hatia mwaka 2021.

Jumatatu, Zuma mwenye umri wa miaka 81 alikuwa mahakamani mjini Johannesburg wakati mawakili wakijadi kesi hiyo.

“Ikiwa raia wanataka niwe rais, nani atawazuia?”, Zuma aliwambia wafuasi wake baada ya kesi kusikilizwa. “ Niruhusu niende na nimalizie kile nilichokianza.

Afrika Kusini inafanya uchaguzi mkuu tarehe 29 Mei ambao unatarajiwa kuwa uchaguzi wenye ushindani mkali tangu ujio wa demokrasia mwaka 1994.

Chama tawala cha African National Congress kinakabiliwa na changamoto katika kura ya maoni na kuna hatari kipoteze wingi wa wabunge tangu kumalizika kwa utawala wa kibaguzi, kutokana na uchumi dhaifu na madai ya ufisadi na usimamizi mbaya.