Mahakama Kuu Kenya yaendeleza marufuku dhidi ya ushoga

Wananchi wa Kenya wakiwa mahakamani kusikiliza hukumu juu ya ushoga, Nairobi, Kenya, Feb.2

Mahakama Kuu nchini Kenya Ijumaa imeendeleza marufuku dhidi ya ushoga,na hili linafanya adhabu ya kifungo cha miaka 14 jela kwa wale wenye mahusiano ya jinsia mmoja kuendelea kutumika katika taifa hilo la Afrika Mashariki.

Mahusiano ya jinsia moja ni kosa la jinai katika nchi zaidi ya 70 duniani, na karibuni nusu ya hizo ziko Afrika. Afrika Kusini ni nchi pekee ya Kiafrrika iliyoruhusu ndoa ya jinsia moja.

“Sisi tunalikataa ombi lao na kutupilia mbali rufaa hii,” Jaji Roselyn Aburili aliiambia mahakama iliyokuwa imefurika watu katika mji mkuu wa Kenya, Nairobi, akieleza maoni ya majaji watatu wa jopo lake bila ya kutaja majina yao.

“Tumegundua kuwa vipengere vilivyokuwa vinahojiwa haviko kinyume cha katiba, hivyo basi rufaa hii ya pamoja iliyoletwa haina ukweli.

Shirika la habari la Reuters limeripoti kesi hiyo na kueleza kuwa wanaharakati waliokata rufaa kwa ajili ya kuhalalisha ndoa ya jinsia moja wanadai kuwa sheria hiyo inavunja katiba ya Kenya ya 2010 iliyokuwa imeboreshwa, kwa kutoa haki sawa, heshima kwa wote na faragha ya kila raia.

“Tutakata rufaa. Tunatarajia kuwa mahakama ya rufaa itabadilisha uamuzi huu wa makosa ambao kwa maoni yetu ni kandamizi,” amesema Eric Gitari, mmoja wa waliofungua kesi kupinga katazo hilo.

Majaji hao walioanza kusikiliza kesi mwaka 2018, walitupilia mbali madai hayo wakisema katazo la mahusiano ya jinsia moja linakwenda sambamba kwa upana zaidi na maadili ya utamaduni wa Kenya ulioelezwa kwa muhtasari katika katiba yake.