Mwilu alikamatwa na kuachiliwa kwa dhamana Jumanne kwa madai ya kutumia madaraka yake visivyo, kupokea fedha kwa njia isiyofaa na vile vile kukwepa ulipaji wa ushuru.
Kesi yarudi mahakama ya chini
Kutokana na kasoro iliyokuwa kwenye hati za maamuzi hayo yaliyo tolewa Jumatano na Jaji wa Mahakama Kuu Chacha Mwita, kesi hiyo imerudishwa kwa hakimu mwandamizi wa mahakama ya kushughulikia kesi za ufisadi Lawrence Mugambi.
Hakimu ameahirisha kikao hicho hadi Ijumaa, August 31, 2018, wiki hii ambapo hatma ya Jaji huyo itafahamika iwapo atasomewa mashtaka au la.
Mwandishi wa idhaa ya Kiswahili anaripoti kuwa mapema asubuhi Jumatano, Naibu Jaji Mkuu Philomena Mwilu alifikishwa kizimbani katika mahakama ya milimani jijini Nairobi, akiandamana na mawakili wake alieleza mahakama inayosikiliza kesi zinazohusu ufisadi kuwa amewasilisha kesi nyingine katika mahakama kuu.
Kesi nyingine yafunguliwa
Lengo la kesi iliyo wasilishwa mbele ya Jaji Chacha Mwita ni kuwa mashtaka anayotaka kusomewa yana husiana na masuala ya kibiashara wala si ya jinai jinsi yanavyoelekezwa.
Kupitia mawakili wake Okong’o Omogeni na John Khaminwa, Jaji Mwilu anasisitiza kuwa masuala yaliyoibuliwa na Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma Noordin Haji dhidi yake ni mkakati na njama ya kumdhalilisha na kumuaibisha mbele ya umma na hatimaye kumuondoa afisini.
Sababu za upande wa utetezi
Akiwasilisha mbele ya hakimu mwandamizi Lawrence Mugambi, James Orengo ambaye ni mojawapo wa mawakili wa jaji Mwilu, anaeleza kuwa masuala hayo ya kibiashara yaliyoibuka takriban miaka mitano iliyopita hayafai kugeuzwa na kuwa ya jinai na kusababisha kukamatwa kwa jaji
Hata hivyo, afisi ya mkurugenzi wa mashtaka ya umma inasisitiza kuwa jaji Mwilu alikiuka sheria ya kimaadili na uongozi kwa kujiingiza katika harakati zinazoonekana za kifisadi kujinufaisha mwenyewe.
Msingi wa tuhuma hizo
Jaji Philomena Mbete Mwilu anadaiwa kuwa kati ya July 31, 2015, na Desemba 16,2016 akiwa katika jimbo la Nairobi, alikataa kulipa ushuru kwa halmashauri ya ukusanyaji ushuru shilingi milioni 3.6 kwa unununizi wa kipande cha ardhi katika jimbo hilo.
Na kati ya Agosti 15,2013 na Oktoba 23, 2014 katika makao makuu ya benki ya Imperial, ambayo kwa sasa ipo chini ya urasimu, mtaani Westlands jijini Nairobi wakati akiwa jaji wa mahakama ya rufaa alitumia madaraka yake visivyo kujizawadi shilingi milioni 12 kwa njia isiyofaa. Na vile vile kupokea hati za kiusalama za benki hiyo kwa njia tatanishi.
Aidha, Jaji Mwilu pia anadaiwa kuwa kati ya Juni 8 na 27,2016 alishindwa kulipa ushuru kwa halmashauri ya ukusanyaji ushuru shilingi milioni 2.4 kwa ununizi wa ardhi.
Imetayarishwa na mwandishi wetu Kennedy Wandera, Kenya